Asali ya Tanzania: Urithi wa Asili na Fursa ya Kiuchumi
Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa wa maliasili, ikijivunia misitu ya asili zaidi ya 450, maeneo ya hifadhi yenye aina lukuki za mimea, na mandhari ya kuvutia. Miongoni mwa rasilimali hizi muhimu ni sekta ya ufugaji nyuki, inayotuletea moja ya bidhaa adhimu, asali halisi ya Tanzania.
Asali hii si tu bidhaa tamu bali pia ni urithi wa kipekee wa taifa, unaotokana na wingi wa maua zaidi ya 450,000, na kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa aina mbalimbali za asali barani Afrika.
Asali ya Tanzania inazalishwa kutoka kwenye mazingira ya asili yenye misitu mikubwa, mikoko, na nyanda za kijani kibichi. Ustawi wa maua kwa wingi, unaochangiwa na hali nzuri ya hewa, hutoa mazingira bora kwa nyuki kuzalisha asali yenye ladha na harufu tofauti tofauti kulingana na asili ya maua yanayopatikana katika maeneo husika.
Mbali na kuwa chanzo cha lishe bora, ufugaji wa nyuki una mchango mkubwa kwa uchumi wa vijijini. Jamii nyingi zinazojihusisha na ufugaji nyuki hupata kipato cha uhakika kupitia uuzaji wa asali ndani na nje ya nchi. Zaidi ya hayo, Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa asali barani Afrika, ikijivunia asali yenye viwango vya juu vya ubora inayotafutwa na masoko ya kimataifa.
Serikali ya Tanzania, kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa sekta binafsi, imeweka mkakati wa kukuza sekta ya ufugaji nyuki. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa uzalishaji wa asali unafanyika kwa viwango vya kimataifa na kuipa bidhaa hiyo soko pana zaidi. Ili kuhakikisha kuwa asali ya Tanzania inajulikana kwa ubora wake, serikali ilianzisha nembo ya biashara ya asali ya Tanzania, iliyosajiliwa rasmi mnamo 12 Julai 2024 chini ya Sheria ya Nembo za Biashara ya Mwaka 1986. Nembo hii, inayosimamiwa na TANTRADE, imeundwa ili kusaidia wazalishaji wa asali, wasambazaji, na watumiaji kwa kuhakikisha kuwa asali inauzwa ikiwa na viwango vinavyotambulika kimataifa.
Kupitia nembo hii, Tanzania inalinda sekta ya ufugaji nyuki kwa kuhakikisha kuwa bidhaa za nyuki zinakidhi viwango vya ubora, zinatambulika kwa soko la kimataifa, na zinatoa thamani halisi kwa watumiaji. Hii ni hatua muhimu katika kulinda jina na hadhi ya asali ya Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.
Kwa kuwa na asali safi inayotokana na mazingira asilia, Tanzania inayo nafasi kubwa ya kupenya katika masoko makubwa ya kimataifa kama vile Ulaya, Asia, na Marekani, ambako mahitaji ya asali ya asili yanaongezeka siku hadi siku.
Miongoni mwa wadau muhimu katika ukuaji wa sekta hii ni TABEDO, API Support, HEAT,Chama cha Wafugaji Nyuki Pemba (PEBA), na Chama cha Wafugaji Nyuki Zanzibar (ZABA). Ushirikiano wa taasisi hizi unahakikisha kuwa sekta ya ufugaji nyuki inakuwa endelevu na inawanufaisha wazalishaji wa ndani kwa kiwango cha juu.
Kupitia mazingira asilia na mkakati madhubuti wa serikali na wadau wa sekta binafsi, Tanzania inazidi kujidhihirisha kama mzalishaji wa asali bora zaidi barani Afrika, kwa kuwekeza zaidi katika ufugaji nyuki na kuhakikisha bidhaa hii inapata masoko mapya ya kimataifa. Sekta ya ufugaji nyuki inachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa na kuinua maisha ya Watanzania wanaojihusisha na uzalishaji wake.
Jiunge nasi katika mchakato wa kuitangaza Tanzania kama kinara uzalishaji wa asali barani Afrika: Onja ladha ya asili, furahia thamani yake, na unga mkono sekta ya ufugaji nyuki kwa maendeleo endelevu ya taifa letu.