Tanzania kuzindua alama ya asali kuvutia soko la kimataifa
Tanzania ipo mbioni kutambulisha nembo ya asali zinazozalishwa hapa nchini ili kuitambulisha bidhaa hiyo muhimu katika soko la kimataifa na kuwanufaisha wakulima wa hapa nchini na uchumi wa nchi kwa ujumla. Maandalizi kwa ajili ya mpango huu wa uzinduzi tayari yamekamilika, ikiwa ni hatua muhimu pia kukuza hatua zote muhimu za mnyororo wa thamani ya Ufugaji Nyuki kupitia (BEVAC-Beeking Value Chain).
Mpango huu unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa kwa pamoja na Shirika laMaendeleo la Ubelgiji (Enabel) na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC). Kupitia BEVAC, mpango huu unalenga kuboresha uzalishaji wa asali wa hali ya juu, kukuza ongezeko la thamani, na kuimarisha biashara kupitia mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki hapa nchini kupitia hatua zote muhimu kuanzia ufugaji, ulinaji asali, uhifadhi na upatikanaji wa masoko. Mpango huu utazinduliwa na Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana, Waziri wa Utalii na Maliasili mkoani Tabora katika Taasisi ya Mafunzo ya Ufugaji Nyuki mnamo Oktoba 4, 2024.
Uzinduzi huo pia utaenda sambamba na uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya hosteli ya wanawake katika taasisi hiyo ya ufugaji nyuki. Akizungumzia uzinduzi huo, Meneja wa Mradi Bwana Stephen Paul kutoka Enabel alisema: “Uzinduzi wa nembo hii ,mbali ya kuitambulisha asali ya Tanzania katika soko la kimataifa, bali pia ni uthibitisho wa ubora wa asali na nta zinazozalishwa hapa nchini, zikiwa na mchango wa takriban Euro milioni 9.55 kila mwaka.
“Mbali na kutengeneza nembo hii , pia tunaboresha soko la bidhaa zetu za asali na kusaidia maisha ya maelfu ya wafugaji nyuki na wafanyabiashara nchini kote.”, amesema. “Nembo hii inasimamia ubora na inawakilisha ubora wa hali ya juu wa asali ya Tanzania katika masoko ya ndani na ya kimataifa,”
“Hivyo, kama taasisi ya serikali yenye jukumu la kuendeleza biashara ya bidhaa zote za Tanzania, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania (TANTRADE) inasimamia Nembo hii inayomilikiwa na serikali ya Tanzania ili kuitangaza asali yetu kimataifa”
”Hii itakuwa ni ishara ya asali yenye ubora na viwango vya juu kwa watumiaji wanaotafuta bidhaa za asali za Tanzania,” ameongeza. Kwa upande wa Serikali ya Tanzania, Bi. Latifa Khamis, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, alisisitiza umuhimu wa mpango huu kwa ukuaji wa kiuchumi wa Tanzania.
“TANTRADE imedhamiria kuunga mkono wazalishaji wetu wa ndani na kuhakikisha kuwa asali ya Tanzania inatambuliwa na kuthaminiwa duniani kote”,amesema na kuongeza; “Kupitia nembo hii, tunatoa fursa mpya kwa wafugaji nyuki wetu na kuchangia katika malengo ya kukuza uchumi na upanuzi wa masoko.”
Mradi wa BEVAC umekuwa muhimu katika kutoa elimu na mafunzo kwa wafugaji nyuki kuhusu mbinu endelevu, kuwawezesha kufikia viwango vya kimataifa vya usalama, ubora, na ufuatiliaji wa masoko ya kimataifa. Hadi sasa, walufaika 4151 wakiwemo wafanyabiashara 38, wafugaji nyuki 4113 na wauzaji wa nje wengi – wamepata msaada mkubwa, ikiwa ni pamoja na rasilimali na uunganishaji wa masoko, kuwasaidia kustawi katika masoko ya ndani na ya kimataifa.
Lengo la mpango huu pia ni kuangalia namna ya kuboresha maeneo muhimu ya ufugaji nyuki kote Tanzania, ikiwa ni pamoja na Kigoma, Shinyanga, Tabora, Katavi, Singida, na Kisiwa cha Pemba.
Mradi wa BEVAC unahakikisha kwamba faida za mbinu bora za ufugaji nyuki na fursa za masoko zinapatikana zaidi. Hivyo, uzinduzi wa Nembo ya Asali ya Tanzania unaashiria hatua muhimu ya ukuaji wa sekta ya ufugaji nyuki, ikitarajiwa kukuza mara mbili uzalishaji wake kutoka tani 30,000 hadi 60,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025. Hatua hii imeunga mkono maendeleo ya hosteli ya wanawake, ambayo itaongeza idadi ya wanawake wanaojiunga na BTI na kukuza ushiriki wao wa muda mrefu katika sekta ya ufugaji nyuki.
Hii ni kuhakikisha uhamasishaji endelevu na ufugaji nyuki wa kisasa, hasa kwa wanawake vijana. Wakati wa sherehe ya uzinduzi, Waziri wa Maliasili na Utalii ataweka jiwe la msingi kwa ajili ya Hosteli ya Wanawake katika Taasisi ya Mafunzo ya Ufugaji nyuki.