Nembo ya Asali ya Tanzania Itakavyowanufaisha Wajasiriamali Sekta ya Nyuki

Asali ya Tanzania inajulikana kwa ubora wake wa hali ya juu, ladha ya kipekee, na thamani yake kubwa katika soko la ndani na la kimataifa. Serikali kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja kupitia mradi wa kusaidia kukuza mnyororo wa thamani ya ufugaji nyuki (Beekeeping Value Chain Support - BEVAC Project) imebuni Nembo ya Asali ya Tanzania ili kusaidia Wafanyabiashara Wadogo na Kati (SMEs) kuboresha bidhaa zao na kufanikisha upanuzi wa masoko yao.

Nembo ya Asali ya Tanzania” iliidhinishwa rasmi tarehe 12 Julai 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (URT) chini ya Sheria ya Nembo za Biashara ama Huduma ya Mwaka 1986, Kifungu cha 28 (2) na Kanuni ya 50. Kwa mujibu wa sheria hiyo, mlinzi na msimamizi wa nembo ya asali ya Tanzania ni TANTRADE.

Nembo ya asali ya Tanzania ilianzishwa ili kuboresha ubora na ushindani wa asali ya Tanzania katika masoko ya ndani na ya kimataifa. Lengo ni kubuni chapa inayotambulika ambayo itatofautisha asali ya Tanzania na zile nyingine kutoka kwa washindani wetu kimataifa, kwa kuonyesha sifa zake za pekee na asilia. Hii inasaidia watumiaji wa bidhaa kutambua asili au chanzo cha bidhaa au huduma iliyopo sokoni.

Hii chapa asali ya Tanzania ina faida kubwa zaidi kwa wafanyabiashara wadogo na kati, ambao watajisajili kuweza kutumia nembo hiyo. Hii ni kutokana na umuhimu wake katika soko la bidhaa ya asali na bidhaa nyingine zitokanazo na sekta ya ufugaji wa nyuki nchini Tanzania.

Pamoja na faida nyingine, chapa hii inaweza kusaidia kutofautisha bidhaa ya asali na bidhaa nyingine za nyuki, ambazo ni halali kutoka Tanzania. Pia, chapa hii inasaidia kuhakiki bidhaa bora inayokubalika, hivyo kutangaza vyema bidhaa za asali na nyuki kupitia chapa na hivyo kuongeza soko lake kimataifa.

Haki ya kutumia na kuchapisha nembo kwenye bidhaa na vifaa vya masoko

Wafanyabiashara wadogo na wa kati wanaosajiliwa rasmi na kupata nembo ya asali yaTanzania wanapata haki ya kutumia alama hii kwenye bidhaa zao, vifungashio, na nyenzo za masoko kama mabango, vipeperushi, na matangazo. Hii huwasaidia kuongeza uaminifu wa wateja kwani nembo inahakikisha ubora na uhalisia wa asali zao; kutofautisha bidhaa zao sokoni dhidi ya bidhaa zisizo na uthibitisho wa ubora; na kuboresha mwonekano wa chapa na kuvutia wateja zaidi ili kuongeza mauzo.

Kuingizwa kwenye tovuti rasmi ya asali ya Tanzania

Wafanyabiashara wadogo na kati waliosajiliwa wanapata fursa ya kutangazwa kwenye tovuti rasmi ya Asali ya Tanzania, ambapo kampuni au bidhaa zao zinapewa wasifu mfupi unaoelezea historia, aina ya asali wanayouza, na mawasiliano yao; kuweka viunganishi (links) vinawaelekeza wateja moja kwa moja kwenye tovuti zao au mitandao yao ya kijamii, hivyo kuondelea kutangaza biashara zao; pamoja na kutoa fursa ya kushiriki katika kampeni rasmi za kutangaza asali ya Tanzania, zinazosaidia kuongeza soko na ufahamu wa wateja kuhusu bidhaa zao. Tovuti hii mpaka sasa imevutia wanunuzi mbalimbali ikiwemo zaidi ya nchi 15 kutoka Ulaya, Marekani, na Asia.

Fursa za kushiriki maonesho ya ndani na nje ya nchi

Wafanyabiashara wadogo na kati wenye nembo ya asali ya Tanzania hupata taarifa za awali na nafasi ya kipaumbele kushiriki maonesho ya kibiashara kitaifa na kimataifa. Kupitia ushiriki wao katika maonesho haya, wajasiriamali hawa watapata faida mbalimbali ikiwemo: kupata wateja wapya na mikataba ya usambazaji wa bidhaa zao; kuongeza maarifa kuhusu mwenendo wa soko la asali ndani na nje ya nchi; kupata fursa za mtandao wa kibiashara (networking) na wadau muhimu wa sekta ya ufugaji nyuki na usindikaji wa asali nchini na duniani kote.

Kuongeza thamani ya chapa (brand) na bidhaa

Kupata nembo ya asali ya Tanzania kunamaanisha kuwa bidhaa husika za wafanyabiashara wadogo na kati zinakidhi viwango vya kitaifa vya ubora. Hii huongeza thamani ya chapa (brand) na bidhaa, hivyo kuwafanya wateja kuwa tayari kulipa bei takikana kwa bidhaa zilizo na uthibitisho wa ubora; kutanuka kwa biashara kutokana na kuongezeka kwa soko kwasababu ya kuaminika na wateja; bidhaa kuweza kushindana katika masoko makubwa, yakiwemo ya kimataifa.

Kuchangia katika juhudi za kutangaza na kujenga chapa (brand) ya Asali ya Tanzania

Wafanyabiashara wadogo na kati waliosajiliwa wanakuwa sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kutangaza Tanzania kama nchi inayozalisha asali bora. Kupitia matumizi ya nembo hii, wajasiriamali hawa wanachangia kwa kuitambulisha Tanzania kama chanzo cha asali ya hali ya juu; wanasaidia kuimarisha sifa ya asali ya Tanzania kwenye soko la kimataifa, hivyo kuongeza mahitaji ya bidhaa zao; Wanahamasisha wakulima na wafugaji nyuki wengi zaidi kuzingatia ubora wa uzalishaji wa asali.

Mfumo wa ufuatiliaji wa asili na ubora wa asali

Wafanyabiashara waliosajiliwa wanapata faida ya kutumia mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji wa bidhaa, inayowawezesha kuthibitisha asili na ubora wa asali yao. Hii ni muhimu kwa sababu ya: kuhakikisha uwazi kwa wateja ambao wanahitaji kujua asili ya bidhaa wanazonunua; kuwapa wafanyabiashara ushahidi wa ubora wa bidhaa zao, jambo linalosaidia kuimarisha uaminifu wa wateja; kupunguza tatizo la bidhaa bandia sokoni, hivyo kulinda sifa ya biashara zao.

Wajasiriamali waliosajiliwa kutumia Nembo ya Asali ya Tanzania wanapata faida nyingi zinazo boresha biashara zao na kuziwezesha kukua. Kutoka kwenye uaminifu wa wateja, upatikanaji wa masoko mapya, hadi usaidizi wa kitaifa katika masoko ya kimataifa, faida hizi zinatoa msukumo mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati katika sekta ya asali na bidhaa nyingine za ufugaji nyuki. Hii ni fursa muhimu kwa wale wanaotaka kuongeza thamani ya bidhaa zao, kuaminika zaidi sokoni, na kufanikisha upanuzi wa biashara zao kwa mafanikio makubwa.

Previous
Previous

Taratibu zinazosimamia matumizi ya Nembo ya Asali ya Tanzania

Next
Next

Tanzania kuzindua alama ya asali kuvutia soko la kimataifa