Taratibu zinazosimamia matumizi ya Nembo ya Asali ya Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) inasimamia nembo ya asali ya Tanzania, ambayo ni nembo ya biashara iliyobuniwa kwa ajili ya wazalishaji, wasambazaji, na watumiaji wanaothamini asali safi na halisi, inayopatikana kwa kuvunwa kitaalamu ili kukidhi viwango vya kimataifa.

Hii inasimama kama ishara ya dhamira ya nchi katika kuboresha na kuhakikisha ubora na uendelevu wa bidhaa ya asali na bidhaa nyingine za nyuki kutoka nchini Tanzania. Nembo ya asali ya Tanzania ni alama ya ubora na uthibitisho wa asali inayozalishwa nchini.

Ili kutumia nembo hii, wazalishaji na wasindikaji wa asali wanapaswa kufuata na kukidhi vigezo maalum vilivyowekwa na mamlaka husika. Vigezo hivi vinalenga kuhakikisha ubora wa bidhaa, ufuatiliaji wa mnyororo wa thamani, na ulinzi wa haki za watumiaji. Maelezo yafuatayo yanaeleza kwa kina kuhusu vigezo vya kutumia nembo ya asali ya Tanzania.

Cheti cha ithibati na usajili

Wazalishaji wa asali na wasindikaji wanapaswa kusajiliwa rasmi na kupokea ithibati kutoka kwa mamlaka husika kabla ya kutumia nembo ya asali ya Tanzania. Miongoni mwa masharti muhimu ni usajili wa wafugaji nyuki na wazalishaji wa asali. Wafugaji wa nyuki na wazalishaji wa asali wanapaswa kusajiliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) au mamlaka nyingine zinazohusika na uzalishaji wa asali.

Pia, viwanda vya usindikaji wa asali vinapaswa kusajiliwa na kupata ithibati kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Hii ni muhimu kuhakikisha kwamba bidhaa inayotolewa sokoni inakidhi viwango vya ubora wa kitaifa na kimataifa.

Ufuatiliaji wa bidhaa

Wazalishaji na wasindikaji wanaotumia nembo ya asali ya Tanzania ni lazima wawe na mfumo ufuatiliaji wa mchakato mzima bidhaa zao. Mfumo huu unahakikisha kwamba mchakato wa uzalishaji, ukusanyaji, usindikaji, na usambazaji wa asali unaweza kufuatiliwa kutoka kwa mfugaji nyuki hadi kwa mlaji. Ufuatiliaji huu unasaidia katika kudhibiti ubora wa bidhaa; kuzuia asali bandia kuingia sokoni, na kuwezesha mamlaka kuthibitisha asili na usalama wa bidhaa.

Idhini ya kutumia nembo ya asali ya Tanzania

Wazalishaji na wasindikaji wa asali ambao wamekidhi vigezo vya ubora wanapaswa kuomba na kupokea idhini rasmi ya kutumia nembo ya asali ya Tanzania kutoka Mamlaka simamizi ambayo ni Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE). Hii ina maana kwamba nembo haitumiki kiholela bila uthibitisho wa mamlaka husika; wazalishaji wanapaswa kuwasilisha maombi rasmi ya kutumia nembo; na wazalishaji waliopata idhini watafuatiliwa mara kwa mara ili kuhakikisha wanazingatia vigezo vya ubora.

Uthibitishaji na uhakiki wa mtumiaji

Ili kuimarisha uwazi na kuzuia udanganyifu wa bidhaa, kila bidhaa inayotumia nembo ya asali ya Tanzania inapaswa kuwa na mfumo wa uthibitishaji wa kidigitali. Hii inajumuisha msimbo wa maandishi (QR Code), ambapo kila chupa au kifungashio cha asali kinapaswa kuwa na QR Code ambayo watumiaji wanaweza kuitumia kuhakiki maelezo ya bidhaa. Pia, taarifa za bidhaa zitapatikana katika mifumo ya kidigitali ambapo watumiaji wanaweza kuthibitisha chanzo cha asali, taratibu za uzalishaji, na uhalali wa bidhaa hiyo.

Nembo ya asali ya Tanzania ni alama ya ubora na inatakiwa kutumiwa tu na wazalishaji na wasindikaji wanaokidhi vigezo vya ubora na uthibitishaji. Uwepo wa cheti cha ithibati na usajili, ufuatiliaji wa bidhaa, idhini ya matumizi, na mifumo ya uthibitishaji wa kidigitali ni hatua muhimu zinazolenga kuhakikisha kuwa asali inayotumia nembo hii inakidhi viwango vya juu vya ubora. Kwa kufuata vigezo hivi, sekta ya uzalishaji wa asali Tanzania itaendelea kukua na kupata imani kubwa katika soko la ndani na kimataifa.

Previous
Previous

Sifa na maana ya nembo ya asali ya Tanzania katika bidhaa

Next
Next

Nembo ya Asali ya Tanzania Itakavyowanufaisha Wajasiriamali Sekta ya Nyuki